Oct 18, 2013
Home »
Habari kuhusu Afya ya mwili
» SAMAKI: Kitoweo bora kinachokuza akili, kuongeza maisha
SAMAKI: Kitoweo bora kinachokuza akili, kuongeza maisha
Si wengi wetu wanaofahamu umuhimu wa kula samaki mara kwa mara na jinsi kitoweo hiki kilivyo na umuhimu wa kipekee katika afya ya binadamu
Samaki ni kitoweo ambacho kinatajwa na hata kupendwa na wengi, binadamu au wanyama.
Kitoweo hiki kinaelezwa kuwa na mafuta yenye kiambata aina ya Omega 3 yanayomfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi kwa muda mrefu.
Vyakula vyote vinavyozalishwa majini huwa na kiambata aina ya Omega 3 yenye mafuta yanayotakiwa kwa mwili wa binadamu yatokanayo na samaki, yana mbegu maalumu zinazomsaidia binadamu katika ukuaji ambazo pia ni maalumu kwa faida ya mfumo wa ubongo na neva.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu kutokana na kutokuzeeka mapema.
Kwa upande wa Tanzania, watu waliozaliwa na kuishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito ikiwemo kisiwa kama cha Ukerewe na maeneo mengine karibu na maziwa Victoria, Nyasa, Rukwa hata visiwani Zanzibar wamebainika kuwa ni watu wenye akili nyingi na wanaishi kwa muda mrefu ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi kitakwimu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Ushauri Nasaha, Lishe na Afya, Counselnuth, Mary Materu anadhibitisha kuwapo na virutubisho vingi vinavyopatikana katika kitoweo hiki cha samaki iwapo wataliwa kwa wakati mwafaka mara tu baada ya kuvuliwa.
“Samaki wana kiambata aina ya Omega 3 ambayo husaidia katika ukuaji wa binadamu na kujenga ubongo wake vizuri, ndiyo maana watu wanaoishi katika maeneo yaliyozungukwa na maji mengi ‘bahari, mito au maziwa’ ni watu wenye akili nyingi na watambuzi hata kama hajaenda shule na akienda shule hufanya vyema sana darasani kama ni mtoto, angalia watu wanaotoka ukerewe au sehemu nyinginezo,” anasema Materu.
Materu anafafanua kuwa kinamama wajawazito kwa upande wao wamekuwa wakipewa ushauri kutumia kitoweo hicho wawapo wajawazito na kuepuka nyama nyekundu ambayo hata hivyo ni muhimu kwa mama mjamzito kutumia ili kuongeza damu haraka kwa mjamzito.
“Wajawazito wanapaswa kula samaki kwa wingi ili kukuza ubongo wa mtoto, pia ni lazima wale nyama nyekundu ili kuongeza damu kwa uharaka mwilini ila tunawashauri isizidi nusu kilo kwa siku saba,” anasema Materu na kufafanua umuhimu wa Omega 3 kwa wajawazito.
“Omega 3 humsaidia mtoto kukuza ubongo, kutengeneza retina kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.
Pia, humsaidia mama kuzuia matatizo kama kifafa cha mimba na sonono baada ya kujifungua. Njia kuu ya mtoto kupata Omega 3 ni kutokana na vyakula anavyokula mama yake.
Kama mama atashindwa kupata vyakula vya kutosha vyenye Omega 3, basi mtoto atachukua ile iliyoko mwilini mwa mama ambayo mara nyingi iko kwenye ubongo wa mama.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Cyril Masawe anasema samaki wana umuhimu katika afya ya mama na mtoto na iwapo mama hatapata Omega 3 ya kutosha anaongeza hatari ya kupata postpartum depression, ‘mtoto mwenye uzito mdogo’, uchungu wa mapema (preterm labour), ‘mtoto kuzaliwa kabla ya muda’, au kulazimika kuzaa kwa upasuaji.
“Watoto ambao wamepata Omega 3 ya kutosha wameonyesha kuwa na umakini mkubwa na upeo mzuri kuliko watoto wengine. Pia, hukua kwa haraka zaidi kuliko yule ambaye hakupata kiambata hicho na huwa mtunzaji mzuri wa kumbukumbu. Hupunguza matatizo ya kitabia, na kwa watu wazima hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na saratani nyinginezo.
Dr Masawe anasema kuwa Omega 3 inahitajika kwa kila binadamu ili kuendelea kuutunza ubongo na kujiepusha na magonjwa yanayotokana na kukosa madini haya.
“Ni vizuri kupata Omega 3 ya kutosha kupitia mlo wa kila siku. Wakati wa ujauzito mwanamke anashauriwa kupata angalau gramu 250 kila siku na katika kipindi cha mwisho (miezi mitatu ya mwisho) kwa sababu katika kipindi hiki mtoto hutumia asilimia 70 ya Omega 3 kujenga ubongo wake na mfumo wake wa neva.
Wataalamu hao wanaelezea vyanzo vinavyoleta madini hayo kuwa vinapatikana katika samaki na mafuta ya samaki hasa samaki wenye mafuta mengi kama vibua (mackerel), sato, salmon, sangara, dagaa, herring na jodari.
Vyakula vingine vyenye Omega 3
Vyanzo mbalimbali vya habari duniani vimewahi kuripoti kuwa wapo samaki ambao si wazuri sana kuwatumia kwani wana sumu aina ya mercury kwa sababu ya machafuko ya kimazingira, hivyo unaweza pia ukapata Omega 3 kutoka kwenye mayai, mkate, juisi, mboga za majani, canola, alizeti, mafuta ya samaki na vyakula jamii ya mbegu.
Kama utapenda kumeza vidonge vya Omega 3 uhakikishe kwamba havijatengenezwa na maini ya samaki kwani hizi zina asilimia kubwa ya retinol Vitamin A, ambayo imegundulika kusababisha madhara kwa watoto.
Omega 3 iliyotengenezwa kutoka kwa nyama ya samaki na siyo maini ni bora zaidi. Kama huna uhakika ni bora kununua vidonge maalumu vya Omega 3 vilivyotengenezwa kwa ajili ya wajawazito. Inaelezwa na wataalamu kuwa mafuta ya samaki yanaweza kuchanganywa katika vyakula vya mboga mboga ikiwemo za majani na hata katika kachumbari.
Tafiti za kimataifa
Mwaka 2012, wanasayansi kutoka Marekani walifanya utafiti kwa watu 17,478 walio na umri chini ya miaka 64, wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari na maziwa duniani ambao wamekuwa wakila vyakula vya samaki na vyakula vinginevyo vinavyopatikana ndani ya maji.
Utafiti huo uliofanyika kwa miaka minne, uligundua kuwa watu wanaoishi kwa kutegemea vyakula vya kwenye maji huishi kwa muda mrefu na huwa na kumbukumbu nzuri na uwezo mkubwa wa kufikiri.
Hata hivyo iligundulika kuwa watu wanaoishi kwa kutegemea samaki huepuka kupata magonjwa ya akili kwa asilimia 19.
Watafiti hao wanaeleza kuwa samaki hula mimea iliyopo ndani ya maji yenye virutubisho ambavyo husababisha binadamu atakayekula samaki huyo kupata virutubisho adimu kutoka kwa samaki huyo.
Hata hivyo, wanatanabaisha kuwa virutubisho hivyo ni sumu ikiwa binadamu atakula pasipo kupitia kwa samaki.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Georgios Tsivgoulis kutoka Chuo Kikuu cha Alabama, Marekani anasema “Watu wanaokula vyakula vya samaki ni vigumu kupata matatizo ya akili na huwa na akili nyingi zinazoambatana na kuishi kwa muda mrefu, hata hivyo mimea mbalimbali inayoota pembezoni mwa bahari na maziwa ina virutubisho bora kwa afya ya binadamu,” alisema Tsivgoulis.
Anasema samaki ni chakula kinachofanya kazi kwa wepesi zaidi mwilini na kusaidia katika kuhifadhi kazi za utambuzi katika maisha ya binadamu, hata hivyo huwa na virutubisho maalumu ambavyo humfanya binadamu aishi kwa muda mrefu.
Wengine waligundua kwamba ulaji wa mlo unaopatikana pembezoni mwa bahari wakiwamo samaki, husaidia kuondoa tatizo la ugonjwa wa moyo, kupooza na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokufa kwa shinikizo la damu.
Inaaelezwa kuwa watu wenye idadi kubwa ya kiambata aina ya Omega 3 Omega 3 wana uwezekano wa kuishi kwa muda mrefu ukilinganisha na watu wenye upungufu wa madini hayo ambayo hutokana na samaki au mafuta ya samaki.
Watu wazima wenye madini hayo pia wametajwa kuwa katika usalama wa kushambuliwa na magonjwa ya moyo na kupooza na mengine yatokanayo na uzee na hivyo kuweza kuishi kwa muda mrefu zaidi.
Source: MWANANCHI